Wakenya wametawala makala ya 24 ya mbio za nyika duniani baina ya shule yaliyoandaliwa Jumapili katika uwanja wa Ngong racecourse, wakinyakua medali 8 kati ya tisa za kibinafsi zilizoshindaniwa.
Diana Chepkemoi na Phanuel Kipkogei walitwaa ubingwa katika mashindano ya chipukizi chini ya umri wa miaka 18 huku Wakenya waifagia nafasi zote tatu za mwanzo.
Chepkemoi aliongoza mbio za mita 3,400 kutoka mwanzo hadi utepeni akitumoia dakika 10 sekunde 47.8,akifuatwa na Mary Nyaboke,kwa dakika 10 sekunde 51.4,ilihali Dorcas Chepkwemoi akachukua nafasi ya tatu akisajii dakika 10 sekunde 53.4 .
Katika kitengo cha wavulana chini ya umri wa miaka 18 umbali wa mita 5,100 Alphonce Kipkogei amenyakua nishani ya dhahabu,akikata utepe kwa dakika 14 sekunde 39.8.
Kevin Kiprop alishinda fedha kwa dakika 14 sekunde 43.6, huku Nelson Simiren akiridhia nafasi ya tatu akifuatwa na Bernard Kikundi,katika nafasi ya nne.
Mganda Japheth Arapsatya alimaliza wa tano akifuatwa na Osama Er Radoumi wa Morocco katika nafasi ya sita.
Jane Wangari aliwaongoza Wakenya kufagia nafasi nane za kwanza katika mita 2400 chipukizi walio chini ya umri wa miaka 15 akiziparakasa kwa dakika 7 sekunde 40.8,sekunde 27 mbele ya Faith Jeptum, aliyemaliza wa pili huku Claire Cheruto akimaliza wa tatu
Peter Lomuryon alitawazwa mshindi katika mita 3,400m kwa wavulana chini ya umri wa miaka 15 kwa dakika 10 sekunde 18.6 akifuatwa na Bemson Tipapa kwa dakika 10 sekunde 22.5 mbele ya Dan Kibet aliyemaliza wa tatu huku Kenya ikifakamia nsihani zote.
Sheila Chepkosgei alifungua kapu la medali kwa Kenya akiwaongoza wenzake kutwaa nafasi za 1,2 na 3 katika mita 1000 chipukizi wasiozidi miaka 12 akikata utepe kwa dakika 3 sekunde 53.2,akifuatwa na Belinda Chepkorir aliyetumia dakika 3 sekunde 55.1,huku Dorcas Chelangat akiridhia nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 3 sekunde 55.1.
Katika mbio za wavulana mita 1,200 Ezron Kimurgor alitwaa ushindi kwa dakika 3 sekunde 43.5 wakati Benjamin Shikuku akifuatia katika nafasi ya pili kwa dakika 3: sekunde 46.7, huku shaba ikimwendea Mganda Caleb Chasinja Kibet .
Kenya pia ilinyakua nishani zote za timu kwenye mashindano hayo .
Takriban wanafunzi 300 kutoka nchini 19 zilishiriki mashindano hayo yaliyohudhuriwa na Rais William Ruto, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu na Rais wa shirika la kimataifa la mashindano ya shule ISF Laurent Petrynka.
Mashindano hayo yalikuwa yakirejea barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu yaandaliwe Marrakech Morocco mwaka 2000.