Kundi la muziki la Sauti Sol lilitoa tangazo la tamasha mbili ambazo wanapanga kuandaa mwezi Novemba na Wakenya wanaonelea kwamba ni ubaguzi.
Kulingana na tangazo hilo, Novemba 2 wataandaa onyesho la watu mashuhuri katika jamii yaani “VIPs” na Novemba 4 waandae onyesho la kina yahe au ukipenda “Fans”.
Wakenya mitandaoni walionekana kuchanganyikiwa na tangazo hilo wengine wakihofu kwamba kutakuwa na tofauti kubwa kati ya tamasha hizo mbili.
Wanahisi onyesho la watu wa kawaida yaani litakuwa na kiwango cha chini cha ubora ikilinganishwa na onyesho la watu mashuhuri.
Kwenye mtandao wa Instagram, mtumizi mmoja kwa jina itsmorara ameandika, “Hili tangazo linaleta dhana ya barabara ya chini kwa chini ya Pangani.” Barabara hiyo huwa imegawanywa mara mbili, moja ikielekea eneo linalochukuliwa kuwa la matajiri na nyingine ikielekea katikati ya jiji la Nairobi.
Usimamizi wa kundi hilo la muziki bado haujatoa taarifa kuhusu lalama za mashabiki na ada ya kiingilio ya awamu hizo mbili za Solfest.