Serikali imehakikishia wakenya kwamba imejitolea katika kuhakikisha ulinzi wa hali ya juu wa data yao.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Eliud Owalo amesema hakuna chochote ambacho kitaizuia serikali isihakikishe kwamba haki ya kila Mkenya ya usimamizi bora wa data inatekelezwa.
Akizungumza baada ya kufungua afisi ya kamishna wa ulinzi wa data jijini Mombasa, waziri alisema kufikia sasa, huduma za serikali 5,084 zimewekwa kwenye mtandao, serikali inapoendeleza ajenda ya kuboreja mfumo wa dijitali.
Serikali inapanga kuzindua vituo elfu 25, vya WiFi katika masoko na vituo vya mabasi kote nchini kama sehemu ya mpango wake wa kidijitali.
Lengo la serikali kulingana na Owalo, ni masoko ambapo kina mama wanaendeleza biashara na vituo vya mabasi ambako vijana wengi hukita kambi bila shughuli za kuwaletea mapato.
Alisema katika dunia ya sasa, muuzaji bidhaa hahitaji kukutana na mnunuzi.
Mtandao wa WiFi wa bure ulizinduliwa Jumapili katika soko la Marikiti, soko la Akamba huko Changamwe na katika soko la Ukunda huko Diani.
Owalo aliahidi kwamba huduma hiyo itazinduliwa baadaye katika soko la Kongowea.