Huduma ya taifa ya polisi imehakikishia wakenya usalama baada ya ubalozi wa Marekani jijini Nairobi kutoa tahadhari ya uwezekano wa mashambulizi.
Taarifa iliyotolewa Jumamosi inasema kwamba maafisa wa polisi watasalia macho nyakati zote na kwamba maafisa wametumwa nyanjani katika kila eneo nchini kulinda usalama.
Huduma hiyo ilisema pia kwamba inakumbatia mbinu ya makundi ya mashirika mbali mbali ya serikali katika kulinda usalama katika kiwango cha kitaifa, maeneo na kimataifa na wanategemea sana ujasusi.
Polisi wanaomba raia pia kutoa ripoti za watu au vitendo vya kutiliwa shaka karibu na maeneo yao kwa vituo vya polisi vilivyo karibu nao au kwa kupiga simu nambari 112, 991 na 999 au 0800722203 ambazo hazitozwi ada yoyote.
Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi ulitoa tahadhari kwa raia wake walioko Nairobi kuwa macho kwani huenda visa vya mashambulizi na utekaji nyara vikatokea.
Ubalozi huo ulitaja maeneo ambayo raia wa Marekani na watalii wa nchi nyingine hupenda kwenda jijini Nairobi na kote nchini ambayo yanasemekana kulengwa na magaidi kila mara.