Rais William Ruto ametoa ahadi kwa wakenya kwamba mpango wa huduma za Afya kwa wote (UHC), utahakikisha wakenya wanapata huduma bora za afya bila malipo, ikiwa ni pamoja na huduma za magonjwa sugu.
Kiongozi wa taifa aliyasema hayo leo Alhamisi alipoarifiwa na maafisa wakuu wa Afya wakiongozwa na waziri wa Afya Susan Nakhumicha na katibu katika wizara hiyo Mary Muthoni, kuhusu utekelezwaji wa mpango huo wa UHC.
“Mpango wa UHC ni ahadi kuu katika Manifesto yetu. Mpango huo unalenga kuhakikisha wakenya wote wanapata huduma bora za afya bila malipo, ikiwa ni pamoja na matibabu ya magonjwa sugu,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto alisema serikali imebuni hazina tatu kugharamia mpango wa afya kwa wote UHC.
Kulingana na Rais, hazina hizo ni pamoja na hazina ya huduma za Afya za kimsingi, hazina ya bima ya afya kwa jamii na hazina ya huduma za dharura na magonjwa sugu.
Aliwahimiza wakenya kujisajili kwa hazina ya bima ya afya kwa jamii SHIF.
Kuanzia mwezi ujao , wakenya watahitajika kutembelea vituo vya afya walivyovijachua kupokea matibabu.