Kenya inatarajia kuzoa medali ya kwanza Juamtatu usiku kwenye makala ya 33 ya Michezo ya Olimpiki inayoendelea jijini Paris Ufaransa.
Bingwa mara mbili wa Olimpiki Faith Kipyegon,mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mita 10,000 Beatrice Chebet,Margaret Chelimo na bingwa wa dunia wa mita 800 Mary Moraa, watajitosa uwanjani jijini Paris Ufaransa.
Kipyegon ,Chebet na Chelimo watashiriki fainali ya mita 5,000 Kenya ikiwinda dhahabu ya pili katika historia ya Olimpiki.
Wakenya watakabiliwa na upinzani kutoka kwa bingwa mtetezi Sifan Hassan wa Uholanzi na mshikilizi wa rekodi ya dunia Gudaf Tsegay kutoka Ethiopia.
Fainali hiyo itaanza kutifua vumbi saa nne na robo usiku.
Kenya ilishinda dhahabu ya kwanza ya Olimpiki mwaka 2016 jijini Rio De Janeiro, kupitia kwa Vivian Cheruiyot.
Baadaye saa tano kasoro dakika 13 kutakuwa na fainali ya mita 800 wanawake, Moraa akiwa mshiriki pekee kutoka Kenya.
Moraa atakuwa na kibarua kigumu cha kuwa Mkenya wa pili kutwaa dhahabu ya Olimpiki tangu Pamela Jelimo aibuke bingwa mwaka 2008 mjini Beijing China.