Home Habari Kuu Wakenya kulipia magari yao ushuru

Wakenya kulipia magari yao ushuru

0

Mswada wa kifedha wa mwaka 2024 unapendekeza ada mbali mbali ambazo wakenya watatozwa na kati ya matozo hayo ni ushuru wa gari. Kila mmiliki wa gari atalipa asilimia 2.5 ya thamani ya gari lake.

Kiwango cha chini cha tozo hilo ni shilingi elfu tano na cha juu kabisa ni shilingi laki moja.

Kampuni za bima ya magari ndizo zimetwikwa jukumu la kukusanya matozo hayo na kuyawasilisha kwa serikali katika muda wa siku tano baada ya kutoa bima.

Adhabu kwa kampuni za bima zitakazokosa kukusanya na kuwasilisha matozo hayo ni faini ya hadi asilia 50 ya ushuru ambao haukukusanywa na kiwango kamili cha pesa hizo.

Magari ya kubebea waginjwa, yanayomilikiwa na serikali kuu, ya serikali za kaunti, ya jeshi la Kenya, ya polisi na ya huduma ya kitaifa ya ujasusi pamoja na ya watu wasiotozwa ushuru hatatozwa ushuru huo.

Mapendekezo hayo ya ushuru yanajiri wakati ambapo serikali inatafuta kuongeza kiwango cha pato la kitaifa ili kufadhili mipango mbali mbali ya maendeleo.

Mkate huenda ukaongeza bei kwa shilingi 10 iwapo mswada huo utapitishwa kwani unapendekeza ushuru wa thamani wa asilimia 16 kwa bidhaa hiyo inayopendwa na wengi.

Wanaopenda mvinyo pia wataathiriwa na ongezeko la bei iwapo mswada huo utapitishwa.

 

Website | + posts