Home Kaunti Wakazi waandamana kulalamikia unyakuzi kwa msitu wa Marmanet

Wakazi waandamana kulalamikia unyakuzi kwa msitu wa Marmanet

Wakazi wa kijiji cha Maina kinachopakana na msitu wa Marmanet katika kaunti ya Laikipia walifanya maandamano barabarani kulalamikia kile walichokitaja kuwa uvumi kwamba msitu huo utagawiwa watu binafsi.

Wanataka majibu kuhusu usemi huo kwani ardhi ya msitu huo ni mali ya serikali.

Watu hao waliokuwa wamejawa ghadhabu walilaumu maafisa wa serikali kuu katika eneo hilo kwa kutotoa kipaumbele kwa masuala ya unyakuzi wa ardhi.

Wanadai kwamba wanyakuzi hao sio wakazi wa eneo hilo lakini wamekua wakionyesha vyeti vya umiliki wa ardhi hiyo wakisema wao ndio wamiliki wa ardhi hiyo ya msitu.

Dorcas Nyokabi, mmoja wa wakazi alielezea wanahabari kwamba walipatiwa haki ya kutekeleza kilimo ndani ya msitu huo huku wakiutunza na hatua ya kuwataka kuondoka eneo hilo ni ya kushtua kwao.

Nyokabi aliongeza kusema kwamba juhudi zao za kuwasiliana na masoroveya wa serikali ili watatue tatizo hilo hazikuzaa matunda.

Anasema wanakijiji wenza wamekamatwa na polisi kwa kile kinachosemekana kuwa kushambulia watu hao wanaodai umiliki wa ardhi hiyo na wanahisi ni njama tu ya kuwajaza woga waache kufuatilia suala la ardhi hiyo.

Mkazi mwingine kwa jina John Thumbi naye alisema wataendelea kupigania haki yao na sasa wanaomba serikali ya kitaifa iingilie kati.