Home Kaunti Wakazi wa Turkana wahimizwa kutunza maeneo Chepechepe

Wakazi wa Turkana wahimizwa kutunza maeneo Chepechepe

Gavana huyo alisisitiza kujitolea kwake katika utunzi wa maeneo chepechepe.

0

Gavana wa kaunti ya Turkana Jeremiah Lomurkai, ametoa wito wa utunzaji bora wa maeneo maeneo chepechepe, ili kuimarisha uwezo wa maeneo hayo kuwa chanzo cha maisha yao na kuboresha viumbe hai.

Akipongeza juhudi ambazo zimechukuliwa katika kuzuia athari za mabadiliko ya tabia nchi na serikali katika upanzi wa miti, Gavana huyo alisisitiza kujitolea kwake katika utunzi wa maeneo chepechepe.

Gavana huyo alifichua kuwa serikali ya kaunti ya Turkana imeshirikiana na mashirika mengine katika kutumia uwezo wa ziwa Turkana kwenye sekta ya utalii, usafiri wa majini na michezo.

“Tunafuraha kuwa NEMA, KFS, KEFRI, KWS, KMA, World Vision, KDF, TUC, LOKADO, KMTC, mradi wa BOMA, Wetland International, na washirika wengine wengi wameonyesha nia ya kufanya kazi na Kaunti kuhusu hatua za kuhifadhi mazingira, ili kulinda mazingira ya maeneo chepechepe dhidi ya uharibifu,” Gavana aliongeza.

Serikali ya Kaunti ya Turkana iliadhimisha siku ya Maeneo Chepechepe duniani 2024, ambayo huadhimishwa kila tarahe mbili Februari ili kukumbuka mkataba wa Ramsar mwaka 1971, uliohimiza utumizi bora wa mfumo hai wa maeneo chepechepe na raslimali zake.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Elizabeth Loote, ambaye ni waziri wa Utalii, Utamaduni, Maliasili na Mabadiliko ya tabianchi, gavana huyo alipongeza mchango wa wakazi wanaoishi kwenye maeneo chepechepe na hali ya uchumi wa kaunti.

Gavana Lomurkai alisema kuwa ziwa Turkana, Mto Turkwel, Mto Kerio na kinamasi cha Lotikipi kuwa maeneo chepechepe kuu ya kaunti ya Turkana na kusisitiza umuhimu wao kuwa vyanzo vya maji, uchumi samawati, utalii na uvuvi.

Loote, alisisitiza kuwa siku hiyo ilikuwa ya kutoa uhamasisho kuhusu maeneo chepechepe chini ya kauli mbiu “Maeneo chepechepe na ustawi wa binadamu”.

Loote, aliongeza kuwa maeneo chepechepe ambazo gavana alizungumzia inakalia eneo kubwa na ina uwezo wa kukidhi mahitaji ya taifa kwa miaka 70.

“Ni muhimu pia kuelewa kwamba maeneo chepechepe huadhirika sana wakati wa ukame wa muda mrefu na hali ya hewa isiyotabirika. Kuna haja ya kukumbatia mbinu mahiri za hali ya hewa ili kukabiliana na uharibifu wa mifumo ikolojia ya ardhioevu,” Waziri alikariri.

Waziri Loote aliwaongoza wakazi katika usafishaji wa mji wa Kerio na kuwahamasisha umuhimu wa utumizi bora wa raslimali.

Maadhimisho kama hayo yalihadhimishwa katika maeneo mbalimbali nchini Kenya, sherehe kubwa ikiwa katika bwawa la Timboroa ambapo waziri wa Mazingira Soipan Tuya aliwarai wale ambao wamejenga makazi kwenye maeneo chepechepe waondoke kwa hiara.

Wageni wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Ofisa Mkuu Joseph Ekalale (Maliasili na mabadiliko ya tabianchi), na Evans Lomodei (Ufugaji wa samaki), Wakurugenzi kutoka Kaunti na waakilishi wa washirika.

Alphas Arap Lagat
+ posts