Familia, marafiki, na wanajamii walikusanyika kumuaga mtoto mdogo prince njoroge gitau, mvulana wa miaka mitano aliyeuawa kikatili na fisi katika kijiji cha flat, Nyacaba huko Juja, kaunti ya Kiambu.
Njoroge, ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la PP1 katika shule ya msingi ya legacy, alishambuliwa na fisi.
Wakiongea baada ya ibada ya mazishi, wanajamii, wakiongozwa na Francis Mwangi, wametoa wito kwa shirika la huduma za wanyamapori nchini KWS kuwakamata fisi hao mara moja, kwani wameendelea kutishia maisha ya wakazi wa kijiji cha flat na eneo zima la juja.
Francis Muiruri mmoja wa wakazi aliwataka viongozi wa kaunti ya kiambu kushirikiana na wakazi wanaokodisha ardhi yao kwa wachimbaji mawe. Alihimiza kuundwa kwa mikakati ya kujaza machimbo baada ya uchimbaji wa mawe ili kuepusha majanga ya baadaye.
katika kujibu hali shirika la KWS limeanzisha kambi katika kijiji hicho na operesheni inayoongozwa na mkurugenzi msaidizi Joseph Dadacha inaendelea kwa lengo la kukamata fisi hao hatari.
Wiki iliyopita wakazi wa Nyacaba walifunga barabara kuu ya thika kwa takriban saa mbili, wakiandamana kupinga kifo cha mtoto huyo.
Maandamano hayo yalidhihirisha kuchoshwa kwa wakazi na uwepo wa wanyama hatari, ambao wamesababisha kifo cha mtoto mdogo na kuvuruga amani katika eneo hilo.
Waziri wa utalii, Rebeca Miano, anatarajiwa kuzuru eneo la juja kesho ili kutathmini hali hiyo.