Home Kaunti Wakazi wa Meru wapokea huduma za matibabu bila malipo

Wakazi wa Meru wapokea huduma za matibabu bila malipo

Wakazi wa kaunti ya Meru wapatao 150 wamefaidika na huduma za bure za afya kama vile matibabu ya macho, kisukari na magonjwa mengine kwa hisani ya chama cha “Lions club of Kenya”.

Akizungumza wakati wa kliniki hiyo ya bure katika ukumbi wa kanisa Katoliki mjini Meru, mbunge wa Imenti kaskazini Rahim Dawood alihimiza wakazi kutumia fursa ya huduma kama hizo za bila malipo kufanyiwa vipimo vya kiafya.

Rahim aliomba chama cha Lions na mashirika mengine kuandaa kliniki kama hizo kwa wingi katika kaunti ya Meru akiongeza kusema kwamba taifa lenye afya ni jamii yenye manufaa.

Simon Njoroge ambaye ni gavana wa pili wa chama Lions wilaya ya 411A alisema kwamba wagonjwa watakaohitaji upasuaji wa macho watapatiwa rufaa hadi Nairobi ambako watapata huduma hizo.

Njoroge naye alihimiza watu wa eneo hilo kutumia vyema kliniki za bila malipo akisema kwamba chama cha Lions kitakuwa kikitoa huduma hizo mara moja kila mwezi katika kaunti zote nchini.

Mathew Kimani rais wa tawi la Kiambu la chama cha Lions alisema wikendi ijayo wataandaa mchakato sawa katika kaunti ya Kiambu.

Website | + posts
Jeff Mwangi
+ posts