Home Habari Kuu Wakazi wa Kisumu kunufaika na mpango wa bima ya afya

Wakazi wa Kisumu kunufaika na mpango wa bima ya afya

Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o, alisema kuwa mpango huo unalenga kuongeza idadi ya watu walio na bima ya afya katika eneo hilo kwa minajili ya kuimarisha afya ya jamii.

0
Gavana wa Kisumu Prof. Peter Anyang Nyong'o.

Serikali ya kaunti ya Kisumu imezindua mpango wa bima ya afya ya bei nafuu, huku ikiwalenga walio kwenye sekta isiyo rasmi.

Mpango huo ambao umepewa jina ‘MARWA’ utashuhudia serikali ya kaunti ikichangia kiwango fulani cha fedha kwenye shilingi 500 ya bima ya NHIF, huku zilizosalia zikichangiwa na wanaonufaika.

Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o, alisema kuwa mpango huo unalenga kuongeza idadi ya watu walio na bima ya afya katika eneo hilo kwa minajili ya kuimarisha afya ya jamii.

Alisema mpango huo umeanzishwa kwa minajili ya kupunguza changamoto zinazokumba walio katika sekta isiyo rasmi, ambapo huwa wanalipa shilingi 500 kwa hazina ya NHIF.

“Tumeanzisha mpango huu ili kukabiliana moja kwa moja na changamoto ambazo watu hawa wamekabiliana nazo. Leo, tunazindua Mpango wa Ruzuku ya Bima ya Marwa, kuruhusu watu binafsi katika sekta isiyo rasmi ambao hawana uwezo wa kumudu malipo ya Shilingi 500,” alisema Gavana huyo.

Aliongeza kuwa sekta isiyo rasmi imeitikia vyema mpango huo, na kuongeza kuwa wakati wa majaribio ya mpango huo, wafanyabiashara 194 katika soko la Kibuye, walijiandikisha na wanafaidika.

“Wachuuzi waliosajiliwa pia walionyesha kujitolea kwao, kwa kulipa nusu ya malipo yanayohitajika. Mbinu hii inayolengwa inakubali mahitaji ya kipekee ya huduma ya afya ya vikundi hivi, kuhakikisha wanapata huduma maalum na usaidizi, “alisema.

Alisema kuwa walio nufaika watawekwa katika mpango wa hazina SHIF wakati utakapokuwa rasmi.

Hadi sasa, wakazi 47,973 wamesajiliwa katika mpango wa NHIF huku serikali ya kaunti ikiwalipia kiasi cha pesa hizo.

Waziri wa Afya kwenye kaunti ya Kisumu Dkt. Gregory Ganda, alisema kuwa watu wote kwenye sekta isiyo rasmi wamehamasishwa kwa minajili ya kuleta mafanikio chanya katika mpango huo.

Aliongeza kuwa idara hiyo imekuwa ikizungumza na walengwa na idara ya fedha ili kujumuisha ada ndogo ya ushuru wa kila siku inayolipwa kwa serikali ya kaunti, ambayo nayo itatumika kulipa sehemu ya malipo.

“Tunachosema ni kwamba, ikiwa mchuuzi analipa Sh30 kwa siku, anaweza kulipa Sh50 na pesa za juu itatumika moja kwa moja katika kulipia hazina ya afya,” alielezea.

Mpango huo umesajili watu 39,720 ambao wametembelea kliniki mbalimbali.