Home Kaunti Wakazi wa Ganze, Kilifi watishia kuua tembo

Wakazi wa Ganze, Kilifi watishia kuua tembo

0

Wakazi wa eneo la Ganze katika kaunti ya Kilifi wametishia kuwaua tembo wanaorandaranda katika eneo hilo na kuharibu mimea. 

Wakiongozwa na mbunge wao Kenneth Kazungu, wamesema wamevumilia kwa muda mrefu na sasa wamechoka.

Kazungu alisema wakazi walikuwa wamepanda mahindi kwenye mashamba yao ili kujihakikishia usalama wa chakula baada ya kunyesha kwa mvua lakini mimea yao sasa imeharibiwa na wanyama hao kutoka Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo Mashariki wanaokwepa na kurandaranda vijijini.

“Tulikuwa na mvua ya kutosha msimu huu na kila mtu alielekea shambani kupanda mahindi yake kama njia ya kuhakikisha usalama wa chakula. Kwa bahati mbaya, kundi la tembo ambao hawajawahi kuonekana katika eneo hili wamevamia mashamba yetu ya mahindi, kuyaharibu kabisa na kutuacha bila chochote,” alisema mbunge huyo.

Aliongeza kuwa kama viongozi, walitoa wito wa kuongezwa kwa ushikaji doria lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Nataka kumuuliza Waziri wa Utumishi wa Umma na Jinsia Aisha Jumwa kuzungumza na mwenzake wa Wanyama pori kuhakikisha kuna fidia ya kutosha kutoka kwa serikali kwa wakulima wetu. Hili lisipofanyika, tutawaua tembo kulipiza kisasi kutokana na kuteseka kwetu kwa muda mrefu.”

Akizungumza wakati wa mpango wa pamoja wa usambazaji chakula cha msaada kutoka kwa serikali ya kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa katika eneo la Bamba, Waziri Jumwa aliahidi kufuatilia suala la fidia ili fedha za kutosha zitolewe kwa jamii hiyo.

Alikosoa fedha chache zilizotolewa na wizara kama fidia kutokana na mzozo kati ya binadamu na wanyama pori akizitaja kuwa ukosefu mkubwa wa haki kwa wakazi wa eneo hilo.

“Naambiwa wanalipa shilingi nane kwa kila mhindi ulioharibiwa. Hii si haki. Nitafuatilia na Waziri mwenzangu na wasipoongeza kiwango cha fidia, basi nitaungana nanyi katika azimio lenu la kuwaua tembo ili Waziri aje mwenyewe kuangazia suala hili.”

Mpango wa usambazaji chakula uliyalenga maeneo yaliyopo katika kaunti ndogo za Ganze, Kaloleni na Magarini ambapo Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro alitoa msaada wa mifuko ya unga wakati serikali ya kitaifa ikitoa magunia ya mchele na maharagwe kwa wakazi ili kuwakinga dhidi ya makali ya njaa.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here