Baadhi ya wakazi wa eneo la Gathaara huko Kinangoo kaunti ya Nyandarua wamewasilisha malalamishi yao kwa idara ya Makavazi ya Kitaifa kuhusiana na kile wanachokitaja kuwa njama ya kufuja fedha za umma.
Wanasema mpango wa kujenga makavazi ya Maumau mjini Olkalou uliotangazwa na Gavana Kiarie Badilisha unakinzana na agizo la Rais William Ruto la kukarabati mahakama ya kikoloni ya Kinyahwe ili kuifanya makavazi ya mashujaa.
Wakati wa mazishi ya shujaa wa Mau Mau Mama Mukami Kimathi yapata miezi mitano iliyopita, Rais William Ruto alikubali ombi la kuwepo kwa makavazi ya Mashujaa na kutangaza kutengwa kwa shilingi milioni 50 kwa mradi huo.
Baadaye, kamati maalum ilizuru eneo la Kinangop kubuni mikakati ya kutekeleza ukarabati huo.
Wakati wa sherehe za siku ya utalii ulimwenguni, Gavana Badilisha naye alitangaza ujenzi na ukarabati wa maeneo ya kuvutia watalii ikiwemo makavazi mjini Olkalou.
Wakazi wa eneo la Kinangoo wanadai pia kwamba eneo lao linabaguliwa kimaendeleo.