Wahudumu wote wa afya katika kaunti ya Meru wametishia kugoma kuanzia Agosti Mosi 2024.
Viongozi wa vyama mbali mbali vya wafanyakazi wa sekta ya Afya waliozungumza nje ya afisi ya gavana wa kaunti ya Meru walilaumu serikali ya kaunti kwa kuwahadaa na kukataa kutekeleza yaliyomo kwenye mkataba wa kurejea kazini wa mwaka jana.
Katibu mkuu wa chama cha maafisa tabibu KUCO George Gibore alielezea kwamba walikutana na maafisa wa serikali ya kaunti ya Meru leo na kuambiwa kwamba hakuna mgao wa bajeti wa kuwapandisha vyeo wahudumu wa afya.
Wahudumu hao wa afya wametishia kuandamana hadi bunge la kaunti ya Meru kutafuta kuangaziwa kwa mambo yao na kujumuishwa kwa mambo hayo kwenye bajeti.
Viongozi waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Elias Mutuma wa chama cha wanafamasia, Nesbit Mugendi wa chama cha wauguzi KNUN, George Gibore wa KUCO na Dennis Mugambi wa chama cha KMPU.
Afya ni mojawapo ya majukumu ya serikali yaliyogatuliwa na jukumu hilo linasimamiwa na serikali za kaunti.
Kaunti mbali mbali zimekuwa zikikabiliwa na migomo ya maafisa wa sekta ya afya kutokana na kile wanachokitaja kuwa kukosa kwa serikali za kaunti kulipa mishahara na hata kuwapandisha vyeo.