Home Kimataifa Wahudumu wa afya Machakos watoa ilani ya mgomo

Wahudumu wa afya Machakos watoa ilani ya mgomo

0
kra
Wahudumu wa afya katika kaunti ya Machakos wametoa ilani ya siku sita ya kugoma iwapo serikali ya kaunti haitakuwa imeshughulikia matakwa yao ya kikazi.
Wahudumu hao walikuwa wametoa makataa ya wiki tatu kwa usimamizi wa kaunti kushughulikia mazingira yao ya kikazi ikiwemo kupandishwa ngazi, nyongeza ya mshahara na kuhakikisha hospitali ina vifaa tiba vya kutosha badala ya wagonjwa kutumwa nje kuvinunua, masuala wanayosema hayajaangaziwa.
Wakiongozwa na Charles Okumu ambaye ni mwenyekiti wa chama cha madaktari nchini, KMPDU ukanda wa Lower Eastern, wanasema imekuwa vigumu kuwaeleza wagonjwa kuwa baadhi ya vifaa havipo hospitalini na kutumwa kwao kwenda nje kuvinunua haistahili kwa kuwa ni hospitali ya umma kando na kuwa gharama ya maisha imepanda.
Pia wanakiri kuwa ukosefu wa wahudumu wa afya wa kutosha katika hospitali za Machakos ni jambo ambalo limewasukuma wengi kufanya kazi kwa muda mrefu na hivyo kuwa kizingikiti katika kushughulikia wagonjwa kwa haraka.
Wameapa kuanza rasmi mgomo wao Jumatatu wiki ijayo ikiwa matakwa yao hayatashughulikiwa.
Kulingana na Okumu, wengi wa wahudumu wa afya wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka kumi ilhali hawajawahi kupandishwa vyeo na sasa wamewaonya wagonjwa kujiandaa kuanza safari ya kupata matibabu kutoka kaunti zingine ikiwemo Nairobi.
Waliyasema hayo wakati wakiwahutubia wanahabari katika hospitali ya Machakos Level 5.
Website | + posts
kra