Home Habari Kuu Wahudumu wa afya hospitali ya Port Victoria wafutilia mbali mgomo

Wahudumu wa afya hospitali ya Port Victoria wafutilia mbali mgomo

0

Wahudumu wa afya katika hospitali ya kaunti ndogo ya Port Victoria katika eneo bunge la Budalangi, kaunti ya Busia wamefutilia mbali mgomo. 

Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama cha wauguzi James Emusugut, wahudumu hao walikubali kurejea kazini baada ya kushiriki mkutano na serikali ya kaunti hiyo na maafisa wa usalama.

Naibu Gavana wa kaunti ya Busia ambaye pia ni Waziri wa Afya Arthur Odera ameipongeza hatua hiyo akiitaja kuwa afueni kwa wagonjwa wengi wanaohitaji mno kuhudumiwa.

Hata hivyo, amewaonya wanaoeneza uvumi kuwa serikali ya kaunti imekosa kusambaza dawa katika hospitali za kaunti hiyo akisema dawa hizo tayari zimesambazwa.

Wahudumu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Port Victoria walisusia kazi kulalamikia kushambuliwa kwa wenzao siku chache zilizopita.

Mshukiwa wa ushambuliaji huo, Vanessa Ogema tayari amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka manne, mashtaka ambayo ameyakanusha.

Ogema ambaye ni mwanafunzi wa teknolojia ya upasuaji katika chuo cha hospitali ya Nairobi Womens aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki mbili baada ya kukanusha mashtaka.

Wadau katika sekta ya afya wamelalamikia visa vinavyoongezeka vya kushambuliwa kwa wahudumu wa afya nchini wakitaka hatua kuchukuliwa mara moja kukabiliana na hali hiyo inayotatiza utoaji huduma.

 

Martin Mwanje & Selyne Wamala
+ posts