Home Biashara Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wahofia hasara

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wahofia hasara

0

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika eneo la North Rift wana hofu kwamba huenda wakajipata katika hali ya mapato yao kupungua pakubwa, kufuatia hatua ya kampuni za kutayarisha maziwa kupunguza kiwango cha maziwa zinazonunua kutoka kwao.

Hali hii inatokana na wingi wa maziwa kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Wakulima hao sasa wanaomba serikali itenge fedha za usawazishaji kwa kampuni ya Kenya Cooperative Creameries ili iweze kununua maziwa yote ya wakulima na kuwakinga kutokana na hasara.

Mvua inayoendelea kunyesha imekuwa baraka kwa wakulima wengi wanaofuga ng’ombe wa maziwa katika eneo la North Rift na imesababisha ongezeko la maziwa.

Mvua hiyo hiyo huenda ikawasababishia matatizo kwa sababu ya ongezeko la maziwa. Kampuni nyingi za kutayarisha na kuuza maziwa zimepunguza bei ambayo zinalipia maziwa kutoka kwa wakulima kutoka shilingi 50 hadi chini ya shilingi 40 kwa kila lita.