Home Kaunti Wafawidhi wa kiadventista watoa taarifa baada ya kanisa kuwapiga marufuku

Wafawidhi wa kiadventista watoa taarifa baada ya kanisa kuwapiga marufuku

0

Waongoza sherehe au ukipenda wafawidhi wa kulipwa wa kanisa la kiadventista nchini wametoa taarifa ya kulaani kitendo cha mfawidhi mwenzao kilichosababisha tawi la kusini mwa Kenya la kanisa hilo kuwapiga marufuku.

Wafawidhi hao kwenye taarifa iliyotiwa saini na Edel Mark kiongozi wa chama cha wafawidhi wa kanisa la SDA, wanasema kwamba wao hufuata kanuni zote za kanisa wanapoongoza hafla mbali mbali kanisani.

“Tukirejelea hafla ya uzinduzi wa albamu ya “Chunya Dwari” ya mwimbaji Lorine Otieno Oktoba 7, 2023, sisi wafawidhi wa kanisa la kiadventista tunalaani vitendo visivyofaa vilivyodhihirika huko.” ndiyo baadhi ya maneno ya taarifa hiyo.

Edel anasema kwamba kulingana na maandiko katika kitabu cha Kutoka 20.8 wanachama wao wana maadili, uzoefu na ni waumini wa kanisa na hivyo hawahusiani na kitendo hicho.

Alimalizia kumkana mfawidhi husika akisema kwamba sio mwanachama wa chama chao na hawamfahamu kamwe.

Usimamizi wa kanisa la SDA kusini mwa Kenya ulitoa taarifa ya kumpiga marufuku mwimbaji Lorine Otieno pamoja na wafawidhi wa kulipwa katika hafla za kanisa.

Usimamizi huo uliondoa pia mamlaka ya maandalizi ya hafla kama hizo za kuzindua nyimbo kutoka kwa viongozi wa kanisa na sasa idhinisho lazima litoke kwa kiongozi mkuu wa kanisa katika eneo hilo.

Wafawidhi wa kulipwa kwenye hafla za kanisani kama harusi, sabato za nyimbo na hafla za pathfinders watakubaliwa tu iwapo wataidhinishwa na bodi ya kanisa na kikao cha shughuli za kanisa.

Haya yote yanafuatia kitendo cha mfawidhi kwa jina Professor Amata maarufu kama Min Jacky cha kusimama kwenye madhabahu akiwa amevaa rinda ilhali yeye ni mwanaume.

Website | + posts