Home Kaunti Wafanyakazi walioachishwa kazi waandamana Eldoret

Wafanyakazi walioachishwa kazi waandamana Eldoret

Wafanyakazi zaidi ya 100 wa kampuni ya Steel Mill mjini Eldoret ambao waliachishwa kazi ghafla wameandamana kulalamikia kile wanachokitaja kuwa kucheleweshwa kwa malipo yao na hatua ya kampuni kutumia maafisa wa polisi kuwafurusha.

Kampuni hiyo iliamua kuwatuta kazi wafanyakazi wake wote kutokana na matatizo ya kiuchumi ambayo yalisababisha ifungwe kwa muda.

Wafanyakazi hao walifahamishwa kuhusu kusitishwa kwa mikataba yao ya kazi na kampuni hiyo na kuahidiwa kwamba wangelipwa pesa ambazo wanadai kampuni hiyo kufikia Jumanne.

Walijikusanya na kwenda hadi kwa majengo ya kampuni hiyo ambapo walipata maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia tayari kukabiliana nao kwa kudai malipo yao ambayo ni jumla ya zaidi ya shilingi milioni 30.

Waliamua kuandamana kwenye majengo ya kampuni hiyo huku maafisa hao wa polisi wakiwatizama kwa mbali.

Msemaji wao kwa jina Michael Omondi, alisema walishtuka kuona maafisa wa polisi ambao walikuwa wamejihami kabisa tayari kupambana na ghasia ndani ya majengo ya kampuni hiyo.