Home Biashara Wafanyakazi wa JKIA kuandaa mgomo kupinga kukodishwa kwa uwanja huo

Wafanyakazi wa JKIA kuandaa mgomo kupinga kukodishwa kwa uwanja huo

0
kra

Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege nchini, KAWU kimetangaza kwamba wanachama wake wataandaa mgomo kulalamikia mpango wa kukodisha Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Wafanyakazi hao wametishia kugoma baada ya miito yao ya awali kwa serikali kusitisha ukodishaji wa uwanja huo kwa kampuni ya Adani kutoka India.

kra

KAWU inasema kwamba serikali haikufuata taratibu zilizoko kwenye katiba katika kuafikia mapatano na kampuni ya Adani kuhusu usimamizi wa JKIA.

Chama hicho kinasema Wakenya hawakuhusishwa katika ukodishaji huo inavyohitajika kikatiba na wafanyakazi wa uwanja huo wa ndege pia hawakuhusishwa.

Katibu Mkuu wa KAWU Moses Ndiema alisema watawasilisha ilani ya siku saba ya mgomo huo leo Jumatatu kwa mamlaka inayosimamia viwanja vya ndege nchini KAA na kampuni zote za usafiri wa ndege.

Ndiema anadai kwamba iwapo uwanja JKIA itakodishwa, wafanyakazi wako katika hatari ya kupoteza ajira kwani kampuni ya Adani inapanga kupunguza idadi ya wafanyakazi.

Seneta wa Kisii Richard Onyonka ndiye alitangaza mpango uliopendekezwa kati ya serikali ya Kenya na kampuni ya Adani wa kukodisha uwanja wa JKIA.

Katika mpango huo, Adani itasimamia JKIA kwa muda wa miaka 30 na baada ya hapo itakabidhiwa kiwango fulani cha hisa kwenye umiliki wa uwanja huo.

Website | + posts