Wafanyabiashara katika masoko ya Muthurwa na Wakulima Nairobi, wamekubali kuhamia soko lililoko katika barabara ya Kangundo siku chache baada ya kupinga hatua hiyo.
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja siku ya ijumaa, aliandaa mkutano na wafanyabiashara wanaouza vitunguu,viazi na mananasi katika juhudi za kutatua mzozo huo kuhusiana na uamuzi wa kaunti hiyo wa kuwahamisha.
Akiongea kwa niaba ya wafanyabiashara, mwenyekiti wa soko la Wakulima Paul Maina, alisema kufuatia mashauriano na Gavana huyo, wafanyabiashara walisadiki kwamba masoko hayo yamekuwa na idadi kubwa ya watu,idadi ambayo ni mara tatu ya ile iliyokusudiwa ya kumudu wafanyabiashara-1,200.
Baada ya kujadiliana na Gavana Sakaja, tumeshawishika kuwa kuna manufaa mengi katika soko lililoko barabara ya Kangundo. Ni la Kisasa na nafasi inayoweza kuwamudu wafanyabiashara 5,000, na tuko tayari kushiriki mpito wa amani,” alisema Maina.
Sakaja alikariri kwamba uhamisho wa wafanyabiashara kutoka soko la Wakulima ni muhimu kwa ajili ya kurejesha utulivu jijini.
“Tuko na nia njema kwa wafanyabiashara wetu na hatuwezi kubali wateseke. Hatua hii itahakikisha kuwa wafanyabiashara wana nafasi nzuri kuimarisha huduma zao,” alisema Gavana Sakaja.
Katika juhudi za kurahisisha mpito, Gavana Sakaja pia alitangaza kuondolewa kwa ulipaji ada kwa muda wa miezi miwili, inayokusanywa na kaunti kutoka wafanyabiashara ili kuwafidia kwa kuvuruga shughuli zao.
Kamanda wa polisi kaunti ya Nairobi Adamson Bungei ambaye pia alihudhuria mkutano huo, aliwahakikishia wafanyabiashara usalama wao wakati wa mpito huku akiwahimiza wadumishe utulivu.
“Lengo letu kuu ni kuhakikisha usalama, na tutatekeleza jukumu hilo,” alisema Bungei.