Home Kimataifa Waendesha mashtaka Uhispania wataka Rubiales afungwe jela

Waendesha mashtaka Uhispania wataka Rubiales afungwe jela

0

Waendesha mashtaka nchini Uhispania wanataka msimamizi wa zamani wa shirikisho la kandanda nchini humo Luis Rubiales wa umri wa miaka 46, afungwe jela kwa miaka miwili unusu kwenye kesi ambapo ameshtakiwa kwa kumbusu mwanasoka Jenni Hermoso mdomoni bila idhini yake.

Wanataka pia kwamba Rubiales, ambaye ameshtakiwa kwa kosa la unyanyasaji wa kingono alipe fidia ya Yuro elfu 50,kwa Hermoso, haya ni kulingana na stakabadhi waliyotuma mahakamani jana Jumatano.

Kisa hicho kilitokea Agosti 20 mwaka jana baada ya Uhispnaia kushinda Uingereza na kuibuka mshindi katika kombe la dunia la wanawake huko Australia, ambapo Rubiales alishika kichwa cha Hermoso na mikono yake miwili na kumbusu kwa lazima kwenye mdomo.

Kamera zilizokuwa zikionyesha matukio ya kutuzwa kwa washindi hao zilinasa kisa hicho na kusababisha malalamiko na kusimamishwa kazi kwa Rubiales na FIFA.

Wakati huo Rubiales alijitetea akisema wote walikubaliana kupeana busu lakini Hermoso wa umri wa miaka 33 akakana.Chini ya sheria za Uhispania, busu kama hilo ambalo halijakubaliwa linachukuliwa kuwa unyanyasaji wa kingono.

Inaripotiwa kwamba Rubiales alijaribu kumshinikiza Hermoso kujitokeza wazi na kutangaza kwamba alikubali kubusiwa suala ambalo waendesha mashtaka wanasema lilimsababishia mchezaji huyo wa kike msongo wa mawazo.

Washirika watatu wa zamani wa Rubiales nao wameshtakiwa kwa kosa la kujaribu kulazimisha Hermoso kukiri kwamba alikubali kubusiwa siku hiyo.

Hermoso alishtaki Rubiales na wenzake mahakamani mwezi Septemba mwaka jana akidai kwamba alisumbuliwa sana aokoe Rubiales wakiwa safarini kutoka Australia na wakati wa likizo ya timu yao huko Ibiza.

Aliomba mahakama pia iamuru kwamba Rubiales asimkaribie na asiwasiliane naye kwa muda wa miaka saba unusu.

Iwapo mahakama itaridhia ombi hilo la waendesha mashtaka haimaanishi kwamba Rubiales atakwenda jela. Sheria ya Uhispania inakubalia majaji kusimamisha kifungo cha gerezani iwapo hakizidi miaka miwili.