Home Kimataifa Waendesha mashtaka katika kesi ya mabwawa ya Arror na Kimwarer washtakiwa

Waendesha mashtaka katika kesi ya mabwawa ya Arror na Kimwarer washtakiwa

0
kra

Mashirika matatu yamewasilisha kesi mahakamani dhidi ya waendesha mashtaka wawili katika kesi ya mabwawa ya Arror na Kimwarer. 

Mashirika ya KHRC, Katiba Institute na Africog yanataka Geoffrey Obiri na Oliver Mureithi wachukuliwe hatua za kisheria kwa kuzembea kazini na hivyo kuvuruga kesi hiyo ya shilingi bilioni 63.

kra

Katika kesi yaliyowasilisha mahakamani Disemba 29, 2023, mashirika hayo aidha yamemshtaki kiongozi wa mashtaka ya umma Renson Ingonga.

Yameitaka mahakama kuondoa kinga ya waendeshaji hao wa mashtaka na kuwawajibisha ikiwa waliokuwa washtakiwa katika kesi hiyo, akiwemo Waziri wa zamani wa Fedha Henry Rotich, watawasilisha kesi mahakamani wakitaka kufidiwa kwa kushtakiwa kimakosa.

Katika kesi hiyo, mashirika hayo yanatafuta kuzuia maafisa wa serikali kutumia fedha za umma kufidia uharibifu ikiwa waliokuwa washtakiwa watashinda kesi dhidi ya kushtakiwa kimakosa.

Isitoshe, mashirika hayo yanaitaka mahakama kuwatoza faini Obiri, Mureithi na Ingonga ili kukatisha tamaa uzembeaji katika wajibu wa uendeshaji mashtaka na hivyo kulinda umma dhidi ya gharama zisizohitajika zinazotokana na vitendo vya watuhumiwa.

Disemba 14, 2023, mahakama ya kukabiliana na ufisadi ilimwachilia huru aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich na washtakiwa wengine wanane kutokana na mashtaka ya ulaghai wa fedha zinazohusiana na ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Mahakama iliulamumu upande wa mashtaka kwa jinsi ilivyoshughulikia kesi hiyo.

Website | + posts