Home Kaunti Wabunge wasaliti wakashifiwa na waandamanaji pwani

Wabunge wasaliti wakashifiwa na waandamanaji pwani

0
kra

Maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 yaliendelea katika kaunti za Lamu na Mombasa siku ya Jumatatu,huku waandamanaji wakiwashutumu wabunge wao kwa kuunga mkono mswada huo.

Katika kaunti ya Lamu, waandamanaji walibeba mabango yaliyokuwa na picha za wabunge ‘wasaliti’ kwa kuunga mkono mswada huo.

kra

Mwandamanaji aliyetambulika kwa jina Mwanaisha Hassan alionyesha ghadhabu zake kwa wabunge hao kuunga mkono mswada huo.

“Tumesikitishwa sana na wabunge wetu waliounga mkono Mswada huu wa Fedha, wametusaliti, tuliwachagua ili wasimamie maslahi yetu, lakini wamechagua kuunga mkono sera zinazotukandamiza,” alisema Mwanaisha.

Mwandamanaji mwingine kwa jina Abdallah Shee alilalamika kuwa Mswada wa Fedha utafanya maisha kuwa magumu kwa wakazi wa eneo hilo ambao tayari wanatatizika kujikimu kimaisha.

“Wabunge wetu wametupa kisogo. Wanatakiwa kuwa sauti yetu bungeni, lakini wametuangusha. Wanafaa wajue kuwa sauti zetu ni muhimu,” alisema Abdallah.

Fatuma Abdalla kwa upande wake alitaka wabunge hao kutoa sababu za kuunga mkono mswada huo.

“Hizi ni sura za usaliti. Hatutasahau kura zao. Wanahitaji kurejea na kutueleza kwa nini walipiga kura ya ndiyo,” alisema Fatuma.

Jijini Mombasa, waandamanaji waliingia barabarani wakipaaza sauti ‘Tumechoka’ wakitaka wabunge wao waliowachagua wawajibike na kuchukua hatua.

Swaleh Abdallah mmoja wa waandamanaji alionyesha ghadhabu zake akisema wamechoka kutumiwa na viongozi.

“Tumechoka kutumika. Sisi sote ni Wakenya, na kama wakazi wa Nyali, maandamano haya ni ya amani. Ukijaribu kutuvuruga Gen Z fanya upendavyo, hakika utatuua. Huu ni mwanzo tu,“ alisema Swaleh.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here