Home Habari Kuu Wabunge wapitisha mjadala wa kuanzishwa kwa hazina ya saratani

Wabunge wapitisha mjadala wa kuanzishwa kwa hazina ya saratani

0
Majengo ya bunge la Kenya

Wabunge hivi leo wamepitisha mjadala wa kuanzishwa kwa hazina ya kitaifa ya matibabu na udhibiti wa ugonjwa wa saratani.

Mbunge wa eneo la Marakwet Magharibi Timothy Toroitich, aliyeleta mjadala huo bungeni aliambia wabunge wenzake kwamba hata ingawa mgao wa bajeti kwa sekta ya afya ni endelevu, hautoshi kugharamia mipango ya kudhibiti na kuzuia saratani kote nchini.

Alitaka mipango hiyo itengewe fedha akisema katiba inatoa haki kwa kila mkenya kupata huduma bora za afya akiongeza kusema kwamba ugonjwa wa saratani ni moja kati ya visababishi vikuu vya vifi nchini.

“Udhibiti wa saratani nchini umelemazwa na ukosefu wa huduma zifaazo na ukosefu wa wataalamu wa kutosha.” alisema mheshimiwa Toroitich.

Kulingana naye, matibabu ya saratani yamefikia kiwango ambapo gharama yake inawazidi wakenya wengi akisema wengi hawakamilishi matibabu kwa sababu hiyo.

Mbunge huyo anasema serikali kupitia kwa wizara ya fedha inastahili kubuni hazina ya kitaifa ya kuzuia na kudhibiti saratani ili kuimarisha mipango ya kuzuia, kudhibiti na kutibu saratani.

Alitetea azma yake akisema sheria ya mwaka 2012 ya kuzuia na kudhibiti saratani iliundwa ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kupima na kutibu saratani na kuhakikisha uwepo wa uwezo endelevu wa kuzuia na kudhibiti saratani.

Website | + posts