Home Habari Kuu Wabunge waombwa kupitisha makadirio ya bajeti

Wabunge waombwa kupitisha makadirio ya bajeti

0

Rais William Ruto ametoa wito kwa wabunge kuunga mkono na kupitisha bajeti yake ya Trilioni 4.2 ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 wakati itafikishwa bungeni.

Akizungumza huko Wote, kaunti ya Makueni jana, kiongozi wa nchi alisema anahitaji wabunge waunge mkono bajeti hiyo ili aweze kutekeleza ajenda yake ya maendeleo.

Ruto aliongeza kusema kwamba viongozi wanastahili kufahamu kwamba siku moja watawajibishwa kwa jinsi walitoa huduma zao kwa taifa hili.

Serikali ya Rais Ruto imeandaa bajeti ya mwaka 2024/2025 ya Trilioni 4.2 ambayo inajumuisha mgao wa serikali za kaunti kulingana na taarifa ya sera ya bajeti ya mwaka 2024.

Bajeti hii ni kubwa ikilinganishwa na ile inayotumika kwa sasa ambayo ni ya shilingi Trilioni 3.6. Serikali inalenga kukusanya bilioni 324 zaidi kupitia ushuru katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2024/25.

Rais William Ruto alikuwa katika uwanja wa Unoa, Wote kaunti ya Makueni kwa ajili ya ibada ya Dayosisi ya kanisa Katoliki jimbo la Makueni.