Home Habari Kuu Wabunge wa Ukambani wataka Kalonzo na Wavinya wachunguzwe kuhusiana na ardhi ya...

Wabunge wa Ukambani wataka Kalonzo na Wavinya wachunguzwe kuhusiana na ardhi ya Mavoko

0

Wabunge wa mrengo tawala wa Kenya Kwanza kutoka eneo la Ukambani, wanataka kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti wachunguzwe na idara ya upelelezi wa jinai DCI kuhusiana na unyakuzi wa ardhi ya umma huko Ukambani.

Wakizungumza kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, wabunge hao walisema wanahurumia waathiriwa wa ubomozi uliotekelezwa kwenye ardhi hiyo wakitaka waliosababisha hali hiyo walazimishwe kuwafidia.

Viongozi hao wanasema wanajua kwamba wahalifu hao wamevamia ardhi nyingine na idara ya DCI inafaa kuchunguza na kuwakamata.

Walisema suala hilo sio la kabila la Kamba bali linahusu kundi la walaghai na viongozi na wale ambao watapatikana na hatia wachukuliwe hatua za kisheria.

Wanataka kwamba mali ya viongozi hao pamoja na walaghai ipigwe mnada na pesa zitakazopatikana zitumiwe kufidia waathiriwa wa ubomozi.

Kwenye taarifa yao kwa wanahabari, viongozi hao walitaka Kalonzo na Wavinya watangaze hadharani wanavyohusiana na mzozo wa ardhi hiyo na ardhi waliyogawiwa kupitia watu wengine.

Tayari idara ya upelelezi wa jinai imetoa orodha ya majina ya watu ambao wanaaminika kuwa na ufahamu kuhusu mzozo wa ardhi hiyo ya kampuni ya saruji ya East African Portland Cement akiwemo mbunge wa eneo la Mavoko Patric Makau.

Watu hao 30 walihitajika kufika kwa afisi ya kuchunguza mizozo ya ardhi katika idara ya DCI leo.

Website | + posts