Home Habari Kuu Wabunge wa kike walalamikia kuchipuka kwa makundi yaliyoharamishwa

Wabunge wa kike walalamikia kuchipuka kwa makundi yaliyoharamishwa

0

Wabunge wa kike wamelalamikia kile ambacho wamekitaja kuwa kuibuka tena kwa makundi ambayo yameharamishwa nchini.

Katika kikao na wanahabari kwenye majengo ya bunge leo, viongozi hao kwenye hotuba ya pamoja iliyosomwa na mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi, waliorodhesha makundi hayo.

Walitaja makundi kama chinkororo, Mungiki, Alshabaab, 42 Brothers, Wakali Kwanza, wajukuu wa bibi kati ya mengine mengi ambayo wanasema vitendo vyao huathiri sana wanawake na watoto.

“Wakati huu wa maadhimisho ya siku 16 za harakati dhidi ya dhuluma za kijinsia tunaambia jamii kwamba tumekuwa tukitumiwa kama ngao ili watekeleze yanayowanufaisha.” alisema Elachi.

Kulingana nao, wanachama wa makundi hayo hutekeleza maovu kama unyanyasaji wa kingono hata mbele ya familia zao, kusimamia kwa lazima magari ya uchukuzi wa umma, kudai ada katika maeneo ya ujenzi, kuuzia vijana dawa za kulevya na mengine.

Lalama zao zinajiri siku chache baada ya lalama za baadhi ya wabunge wa maeneo ya Mlima Kenya kwamba kulikuwa na mipango ya kufufua tena kundi haramu la Mungiki.

Wakati huo, viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Naivasha Jane Kihara, waliandika taarifa kwa vyumba vya habari wakidai kwamba kundi hilo lililotesa watu wa eneo hilo mwanzo wa miaka ya 2000, huenda likarejeshwa tena.

Walisema wao kama kina mama wanakumbuka mashambulizi ya wanachama wa kundi hilo na hawangependa lirejee.

Website | + posts