Wabunge waliochaguliwa kupitia chama cha ODM wamesema kwamba hawahusiki kwa vyovyote na uteuzi wa viongozi wa chama hicho kuhudumu kama mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza.
Katika taarifa baada ya mkutano wa leo asubuhi viongozi hao wamefafanua kwamba wengi wao kama sio wte walihudhuria mkutano wao wa Julai 12, 2024 katika afisi za wakfu wa Jaramogi jijini Nairobi.
Wamesema kwenye mkutano huo kamwe hawakujadili na kukubaliana kwamba baadhi yao wajiunge na serikali ya Rais William Ruto. Wameongeza kusema kwamba ni jambo la kushtukizia kwao pia kwamba viongozi mbali mbali wa chama walitajwa na Rais Ruto kama mawaziri wateule.
Kulingana nao hatua ya viongozi hao wachache inaharibia chama kizima jina ikitizamiwa kwamba kimekuwa kikipigania wananchi ambao hawaridhishwi na utawala wa sasa.
Wabunge hao wa ODM kadhalika wanasema kwamba uteuzi uliofanywa haudhihirishi utofauti wa wanachama wa chama ambacho wanakipenda sana katika kuangazia jinsia, umri na maeneo mbali mbali nchini.
“Tungependa kurejelea msimamo wa katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna kwamba uamuzi wa wanne walioteuliwa mawaziri ni wao binafsi na wala sio wa chama.” walisema wabunge hao katika taarifa.
Kando na hilo, wabunge hao sasa wanataka uongozi wa chama ufanye hala hala kuchagua viongozi wapya wa chama kuchukua nyadhifa za walioteuliwa mawaziri.
“Mwisho marafiki wetu wanne watarajie mahojiano makali kuhusu ufaafu wao wa kuhudumu kama mawaziri nyadhifa walizojitafutia wenyewe, wakati wa usaili bungeni.” wabunge hao walimalizia taarifa yao kwa kauli hiyo.