Home Kaunti Waathiriwa wa mvua kubwa wapokea msaada Nyandarua

Waathiriwa wa mvua kubwa wapokea msaada Nyandarua

Walioathirika na mvua kubwa iliyonyesha katika kaunti ya Nyandarua wamepokea msaada kutoka kwa viongozi wa kaunti hiyo na wahisani wengine.

Mvua hiyo kubwa iliathiri sana wakazi wa eneo la Bongo ambapo familia zipatazo 15 zilipoteza makazi yao.

Wanasema mvua hiyo ambayo ilikuwa imeandamana na upepo mkali iling’oa miti na milingoti ya stima ambayo iliangukia baadhi ya nyumba na ikaua mifugo.

Akizungumza alipozuru waathiriwa, mwakilishi wa afisi ya mbunge wa kaunti ya Nyandarua David Kamunya alisema kwamba familia hizo zinahitaji msaada wa dharura ikitizamiwa kwamba makazi yao yameharibiwa kabisa.

Kamunya alielezea kwamba mbunge wa kaunti ya Nyandarua Faith Gitau aliomba usaidizi kutoka kwa Naibu Rais kwa sababu kaunti pekee haiwezi kufidia uharibifu huo mkubwa.

Kupitia kwa afisi ya Gitau, waathiriwa walipokea nguo na chakula kama msaada wa muda huku suluhisho la kudumu likitafutwa.

Website | + posts
Lydia Mwangi
+ posts