Kundi moja la Muslim World League, limetoa chakula cha msaada na vifaa vingine Kwa waathiriwa wa mafuriko kaunti ya Garissa ambao wanatarajiwa kurejea makwao mwishoni mwa mwezi Januari.
Mafuriko yaliyosababishwa na mvua za El Niño,yaliwaathiri wakazi wengi wa eneo hilo mwishoni mwa mwaka jana, huku baadhi ya wakazi wakirejea kwao na wengine wakikosa kurejea baada ya nyumba zao kuharibiwa.
Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo, Mkurugenzi wa Muslim World League hapa nchini Dkt. Hassan Mohamed Idris, alisema wanatafuta mbinu zingine za kuwasaidia waathiriwa hao ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba mpya baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.
“Kama sehemu ya mpango wetu wa kuwasaidia walioathiriwa na majanga, tumefika hapa kuwasaidia wenzetu walioathiriwa na mafuriko ya mvua za El Nino,” alisema Idris.
Kwa upande wake chifu wa eneo hilo Harat Maalim, alisema waathiriwa wa mafuriko hayo walitoka maeneo ya Ziwani, Bakuyu na Mathengeni, katika eneo la Tana River.