Home Habari Kuu Waathiriwa wa El Nino kuendelea kupokea misaada

Waathiriwa wa El Nino kuendelea kupokea misaada

0

Kituo cha kitaifa cha kushughulikia athari za mvua ya El Nino kimetangaza kwamba misaada itaendelea kutolewa kwa waathiriwa wa mvua hiyo, kikisema kufikia sasa kimesambaza chakula na vifaa vingine.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari kituo hicho kilitangaza kwamba kimesambaza tani 2,279 za mchele, 803 za maharagwe, 7.5 za nyama na 4 za unga.

Kaunti ambazo zimefaidika na msaada huo ni Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu, Tana River, Taita Taveta, Garissa, Wajir, Mandera, Marsabit, Isiolo, Kitui, Meru, Makueni, Tharaka Nithi, Embu, Samburu, Turkana, Busia, Migori, Kisumu, Homabay na Muranga.

Huku kikisisitiza kujitolea kwake kuendelea kushughulikia athari za El Nino, kituo hicho kimetangaza pia kwamba tani 257.5 za dawa zimesambaziwa kaunti hizo kukabiliana na maradhi kama kipindupindu.

Familia zipatazo elfu 94 zimerejea kwenye makazi yao ya awali kufuatia kupungua kwa maji ya mafuriko katika maeneo hayo na kwa sababu hiyo kambi 51 zimefungwa katika kaunti za Mombasa, Wajir, Kitui, Meru, Marsabit, Elgeyo Marakwet, Turkana, Narok, Nyandarua,
Busia na Nairobi.

Huko Tana River mojawapo ya maeneo yaliyoathirika zaidi, wahanga wa mafuriko wamepokea mabati, godoro, blanketi, vifaa vya kimsingi na hema.

Barabara ambazo awali hazikuwa zinapitika katika eneo la Kaskazini Mashariki na Pwani kutokana na athari za mafuriko sasa zinapitika. Madereva hata hivyo wanahimizwa kuwa waangalifu.

Maeneo ya Kusini Mashariki na Pwani yanatarajiwa kupokea mvua wakati wa sherehe za krismasi, huku maeneo ya Kaskazini mashariki na Kaskazini Magharibi yakisalia makavu na mvua ya kiwango cha chini.

Website | + posts