Home Kimataifa Wawaniaji 24 wajitosa katika kivumbi cha Ikulu DR Congo

Wawaniaji 24 wajitosa katika kivumbi cha Ikulu DR Congo

Rais wa taifa hilo Felix Tshisekedi, aliyechukua uongozi wa DRC mwaka 2018, pia alisajili  uwaniaji, akitafuta muhula wa pili wa miaka mitano.

0
Uchaguzi wa urais nchini DRC, utaandaliwa tarehe 20 mwezi Disemba.

Wagombeaji 24 wamejitosa ulingoni kuwania Urais katika Jamhuri ya Kidemkokrasia ya Congo katika uchaguzi wa Disemba mwaka huu.

Hata hivyo wawaniaji hao watasubiri hadi mahakama ya kikatiba itakapoidhinisha majina yao, huku orodha ya mwisho ya wawaniaji Urais ikitarajiwa kutolewa tarehe 18 mwezi Novemba.

Rais wa taifa hilo Felix Tshisekedi, aliyechukua uongozi wa DRC mwaka 2018, pia alisajili  uwaniaji, akitafuta muhula wa pili wa miaka mitano.

“Huku ikizingatiwa kuwa upinzani wa taifa hilo unakumbwa na mianya, Rais huyo mwenye umri wa miaka 60, ana fursa nzuri ya kutwaa ushindi,” alisema mtaalamu wa kisiasa Christian Moleka.

Kulingana na Moleka, upinzani wa taifa hilo unapaswa kushirikiana na kuwa na muwaniaji mmoja, ili kuwa na nafasi ya kumbwaga Tshisekedi.

Miongoni mwa washindani wakuu wa Tshisekedi ni pamoja na mshindi wa tuzo ya Nobel Dkt. Denis Mukwege, mwanabiashara bwanyeye na ambaye alikuwa Gavana wa Katanga, Moise Katumbi, na  Martin Fayulu aliyewania urais mwaka 2018 lakini hakufua dafu.

Hata hivyo, ni mwanamke mmoja  Marie-Josee Ifoku Mputa, aliyejisajili kuwania urais miongoni mwa wawaniaji hao 24, ambaye pia aliwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Mazingira ya kisiasa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekumbwa na wasiwasi, huku upinzani ukisema uchaguzi huo utakumbwa na wizi..

Website | + posts