Wafuasi wa mrengo wa kisiasa wa kulia wamekimbizana na maafisa wa polisi katika sehemu mbali mbali za Uingereza kufuatia kuenezwa kwa habari zisizo sahihi kuhusu kuuawa kwa kudungwa kisu kwa wasichana watatu.
Miji mingi huko Uingereza imekumbwa na maandamano yenye vurugu ya watu wa mrengo wa kulia na wasiopendelea uhamiaji siku chache baada ya taarifa hizo kusambaa.
Iliripotiwa kwamba mshukiwa mkuu wa kisa hicho cha mauaji katika shule moja ya watoto ya densi huko Southport ni mhamiaji muumini wa dini ya kiisilamu.
Hata hivyo maafisa wa polisi wametoa ripoti inayoashiria kwamba Axel Rudakubana wa umri wa miaka 17 ni mzaliwa wa eneo la Cardiff, Wales, lakini waandamanaji wameendeleza harakati zao.
Katika jiji la Liverpool waandamanaji waliwarushia maafisa wa polisi mawe na hata viti huku hali sawia ikishuhudiwa katika jiji lililo karibu la Manchester.
Polisi wa Merseyside waliripoti kwamba maafisa kadhaa wa polisi walipata majeraha wakijaribu kutuliza hali.
Biashara pia hazikusaazwa kwani waandamanaji waliharibu baadhi yazo, wamiliki wasijue la kufanya.
Huko Leeds, watu wapatao 150 waliokuwa wamebeba bendera ya Uingereza walisikika wakiimba nyimbo za kukashifu waandamanaji wengine kwa kutokuwa wa asili ya Uingereza.
Waandamanaji hao pia walisikika wakiwarejelea waliokuwa na bendera kuwa wanachama wa kundi la Nazi na wanafaa kuondoka barabarani.
Polisi jijini Hull waliripoti kutiwa mbaroni kwa watu wanne huku maafisa watatu wa polisi wakijeruhiwa wakidhibiti waandamanaji waliokuwa wakiwarushia chupa na mawe.
Jijini London waandamanaji wengi walikamatwa akiwemo mmoja aliyefanya ishara ya Nazi aliyoelekeza kwa kundi jingine la waandamanaji.
Wasimamizi wa maabadi ya waisilamu nchini humo wamehimizwa kuongeza ulinzi wa maeneo hayo huku serikali ikituma maafisa zaidi wa polisi kujaribu kudhibiti hali.
Waziri mkuu mpya wa Uingereza Keir Starmer anapambana na jaribio lake kuu la kwanza uongozini baada ya kuchaguliwa mwezi mmoja tu uliopita. Amekashifu mrengo wa kulia na kuulaumu kwa vurugu huku akiunga mkono maafisa wa polisi kuwachukulia hatua kali.
Jumamosi Starmer alifanya mazungumzo na mawaziri kadhaa ambapo alisema hakuna kisingizio chochote cha waandamanaji kuzua vurugu.