Waandalizi wa filamu nchini Uganda wana kila sababu ya kutabasamu kufuatia kuanzishwa kwa mpango wa kufufua tasnia ya filamu kwa ajili ya kuboresha mapato katika eneo zima la mashariki mwa Afrika.
Mpango huo unafadhiliwa na kamati ya serikali mbali mbali kuhusu kulinda na kuimarisha tamaduni tofauti ya shirika la umoja wa mataifa kuhusu elimu, sayansi na utamaduni UNESCO.
Uganda pekee imepokea dola elfu 99,960 sawa na shilingi milioni 370 za Uganda kutoka kwa hazina ya kimataifa ya tofauti ya utamaduni.
Ruth Tusasirwe Muguta anayesimamia masuala ya utunzaji wa jamii katika wizara ya jinsia, leba na maendeleo ya jamii aliambia wanahabari kwamba lengo kuu la mpango huo ni kutumia teknolojia ya kidijitali kuchochea ukuaji endelevu na kuboresha mapato katika tasnia ya filamu.
Kando na Uganda, mpango huo utatekelezwa pia kwenye nchi za Rwanda, Tanzania na Ethiopia.
Baada ya filamu kutayarishwa zitachapishwa kwenye majukwaa mbali mbali mitandaoni ambapo zitafikiwa na watu wengi hata nje ya eneo la mashariki mwa Afrika na hivyo kujulikana pakubwa.