Home Habari Kuu Vyuo Vikuu vya Umma mbioni kujiunga na mtandao wa eCitizen

Vyuo Vikuu vya Umma mbioni kujiunga na mtandao wa eCitizen

0

Huduma zaidi ya 1,000 zinazotolewa na Vyuo Vikuu vya Umma hivi karibuni zitapatikana kwenye mtandao wa eCitizen.

Rais William Ruto ametoa makataa ya hadi mwisho wa mwaka huu kwa taasisi zote za umma, vikiwemo vyuo vikuu, kuhamishia huduma zao kwenye mtandao huo.

Makamu Machansela na wasimamizi wakuu wengine wa vyuo vikuu vya umma kutoka kaunti zote 47 nchini kwa sasa wanakutana katika hoteli moja iliyopo eneo la Mlolongo, Athi River, kaunti ya Machakos ili kuhitimisha taratibu za kujiunga na mtandao huo kwa mujibu wa agizo lililotolewa na Rais Ruto.

Mkutano huo ulifunguliwa na Katibu wa Idara ya Uhamiaji na Huduma za Raia Prof. Julius Bitok.

Prof. Bitok alitoa wito kwa wasimamizi hao kutii agizo lililotolewa na Rais na linalokusudia kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

“Tumevuka ng’ambo ile ingine kuhusu suala hili na hatuna budi bali kukumbatia uhamishaji wa huduma mtandaoni. Si suala la kujadiliwa kwamba vyuo vikuu vyote vya umma vinatakiwa kutii agizo hilo na kwa sababu nzuri kwani uwekaji huduma mtandaoni ni lengo la urithi la serikali,” alisema Prof. Bitok.

Huduma zaidi ya 5,000 zinazotolewa na serikali zinapatikana kwenye mtandao wa eCitizen na serikali inalenga kuhamishia huduma zote kwenye mtandao huo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Makamu Machansela waliozungumza wakati wa mkutano huo walitoa wito kwa serikali kupeana intaneti ya bure na ya kutegemewa kwa taasisi za umma ili iwe rahisi na nafuu kwa waliopo vyuoni kufurahia huduma za mtandaoni.

Pia walitaka kuhakikishiwa ikiwa vyuo vikuu vitaweza kupata kwa wakati mwafaka fedha zinazokusudiwa kuendesha shughuli za kila siku na kugharimia matumizi mengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here