Home Habari Kuu Vyama vya ushirika vitachochea ukuaji wa uchumi, asema Rais Ruto

Vyama vya ushirika vitachochea ukuaji wa uchumi, asema Rais Ruto

0

Rais William Ruto amesema Serikali ina nia ya kuimarisha vyama vya ushirika ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Alisema vyama vya ushirika vitasaidia urasimishaji wa wanabiashara na wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi.

Hili, alieleza, litasaidia kuwaleta Wakenya wanaofanya kazi kwa bidii pamoja, kuwawezesha kufaidika na uchumi wa muungano wa viwango.

Alibainisha kuwa vyama vya ushirika pia vina uwezo wa kukuza utamaduni wa kuweka akiba na kuwapa wanachama fursa ya kupata mikopo kwa bei nafuu.

Alizungumza hayo siku ya Jumamosi wakati wa Sherehe za 101 za Sikukuu ya Ushirika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa KICC jijini Nairobi.

Viongozi waliohudhuria ni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Mawaziri Simon Chelugui (Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo na za Kati) na Alice Wahome (Maji na Umwagiliaji), miongoni mwa wengine.

“Tutaweka sera mpya, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo kikuu cha ukwasi, ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCO).”

Rais alisema kuwa hii pia itapunguza hatari za utendakazi zinazovikumba vyama vya ushirika vya akiba na mikopo.

“Mabadiliko hayo pia yatawezesha ukopaji wa muda mfupi baina ya Sacco na kurahisisha ufikiaji wa mfumo wa malipo wa kitaifa,” aliongeza.

Alieleza kuwa Serikali inavisaidia vyama vya ushirika kwa kuanzisha vituo vya kuleta pamoja na kusambaza kwa ajili ya kuhifadhi, kuongeza thamani na masoko ya mazao ya kilimo.

“Lengo la ushirikiano huu ni kupunguza hasara za baada ya mavuno, kuondoa makundi ya wanabiashara walaghai na kuongeza mapato ya wakulima.”

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here