Home Habari Kuu Vyama vya kisiasa vyahimizwa kuwateua wanawake zaidi

Vyama vya kisiasa vyahimizwa kuwateua wanawake zaidi

0

Msajili wa vyama  vya kisiasa Ann Nderitu, ametoa wito wa kuchaguliwa na kuteuliwa kwa wanawake zaidi katika vyeo vya kisiasa, ili kutimiza sheria ya usawa wa jinsia.

Akiongea katika hafla ya ufunguzi wa afisi mpya mjini Garissa, Nderitu alielezea masikitiko yake kuwa eneo hilo halijatilia mkazo uongozi wa wanawake na vijana.

Aliwarai wanaume katika kaunti ya Garissa kuwaunga mkono wanawake ambao wameonyesha ari katika uongozi wa kisiasa ili waweze kuwa na uongozi mpya ikiwa ni njia ya kufikia utawala wa kijinsia wa thuluthi mbili.

”Ninataka kuwasihi wanaume wote kutetea uteuzi na uchaguzi wa wanawake. Wanawake tunaowazungumzia ni mabinti zetu na kila mzazi angetaka binti zao wachaguliwe kuwa viongozi,” alisema Nderitu.

Aidha Nderitu alibainisha kuwa afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa, ni sehemu ya asasi mbali mbali kuhusu jinsia ambayo imewasilisha mapendekezo ya kukagua sheria ya vyama vya kisiasa ili kuruhusu bunge la kitaifa kuwa na sheria ya thuluthi mbili ya jinsia.

“Hivi sasa tuna nia njema ya kisiasa kutoka kwa rais na tuna makubaliano na bunge katika kuibua miongoni mwa mambo mengine suala la utawala wa kijinsia. Kwa msaada wa aina hii, tunaweza kufanyia kazi sheria ya kijinsia ya thuluthi mbili,” alisema.

Alphas Lagat
+ posts