Home Habari Kuu Vurugu zazuka Meru baada ya mkutano wa Gavana

Vurugu zazuka Meru baada ya mkutano wa Gavana

0

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza anataka maafisa wa polisi wachunguze kisa cha jana Jumapili ambapo vurugu zilizuka kwenye mkutano aliokuwa ameandaa katika eneo la Makiri, eneo bunge la Igembe Kusini.

Mkutano huo uliandaliwa chini ya mpango wake kwa jina “Okolea” ambapo alikuwa amepanga kugawa magodoro na kuipatia familia moja ng’ombe wa maziwa.

Baadhi ya wakazi waliokuwa na ghadhabu waliandamana hadi eneo la mkutano ambapo wanasemekana kuchoma magodoro hayo, wakamchinja ng’ombe huyo na kugawana nyama.

Inakisiwa kwamba vurugu hizo zinatokana na mvutano wa muda mrefu ambao umekuwepo kati ya Gavana Mwangaza na naibu wake Isaac Mutuma.

Kijiji cha Makiri ni nyumbani kwa Mutuma na huenda wenyeji walionelea mkutano huo wa usaidizi kuwa kejeli kwa jamii ya eneo hilo.

Maafisa wa polisi walilazimika kutumia vitoza machozi kutuliza hali.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook, Mwangaza aliomba maafisa wa usalama wachunguze kisa hicho na kuchukua hatua dhidi ya waliochochea vurugu hizo.

Alisema pia kwamba hawatasita kuendelea kusaidia jamii katika kaunti ya Meru.

Awali, Mwangaza alikuwa amechapisha picha ambazo zinaonyesha wenyeji wa eneo hilo wakiwa wamepokezwa magodoro na hata mabati, nyuso zao zikiwa na furaha.

Mumewe Gavana Mwangaza, Murega Baichu ambaye ni mwanamuziki anaonekana pia kwenye picha hizo akitumbuiza umati.

Website | + posts