Home Kimataifa Vita vya Israel na Gaza: UN yasema mashambulizi ya Israel hayapungui Gaza

Vita vya Israel na Gaza: UN yasema mashambulizi ya Israel hayapungui Gaza

0

Mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza hayapungui, afisa wa Umoja wa Mataifa ameiambia BBC, baada ya kutembelea hospitali inayotatizika kuwatibu majeruhi.

Gemma Connell wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinadamu OCHA aliiambia BBC kile alichokiona katika hospitali ya Al-Aqsa katikati mwa Gaza Jumatatu ni “mauaji kabisa”.

Watu wengi waliojeruhiwa vibaya hawakuweza kutibiwa kwa sababu hospitali ilikuwa “imejaa kabisa”, alisema.

Waziri mkuu wa Israel hapo awali aliapa kuzidisha mapambano tena dhidi ya Hamas.

Benjamin Netanyahu alisema alitembelea Gaza Jumatatu asubuhi na kwamba operesheni ya kijeshi ya Israel huko “haijakaribia kuisha”.

Kauli yake inakuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kusema Israel inapaswa kupunguza makali ya mashambulizi yake.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) inasema kuwa wanajeshi wa Marekani wamefanya mashambulizi ya anga nchini Iraq dhidi ya “wanamgambo wanaodhaminiwa na Iran” kujibu shambulio katika kambi ya wana anga ya Irbil na kuwajeruhi wanajeshi watatu wa Marekani, mmoja wao vibaya sana.

Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin alisema mashambulizi hayo yalilenga vituo vitatu vinavyotumiwa na Hezbollah na washirika wake.

Amesema kumekuwa na mfululizo wa mashambulizi ya wanamgambo hao katika kambi za Marekani nchini Iraq na Syria, na kusisitiza kuwa Marekani haitasita kuwalinda watu wake na vituo vyake.

Kumekuwa na ongezeko la shughuli za Hezbollah na wanamgambo wengine wenye silaha katika eneo hilo baada ya operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza.