Home Habari Kuu Vita dhidi ya ufisadi: mihimili mitatu ya serikali kushirikiana

Vita dhidi ya ufisadi: mihimili mitatu ya serikali kushirikiana

0

Mihimili mitatu ya serikali ambayo ni serikali kuu, idara ya mahakama na bunge imekubali kushirikiana ili kuimarisha vita dhidi ya ufisadi nchini. 

Hayo yaliafikiwa wakati wa mkutano kati ya Rais William Ruto, Jaji Mkuu Martha Koome na Maspika Moses Wetang’ula wa bunge la Taifa na Amason Kingi wa bunge la Seneti.

“Ufisadi unasalia kuwa tishio kwa taifa ambao umepenyeza hadi mihimili mitatu ya serikali na kudunisha uwezo mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu na kuhujumu mageuzi yanayohitajika mno ya taifa letu,” ilisema taarifa kutoka kwa msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

“Serikali kuu, bunge na idara ya mahakama zinakubaliana kustawisha kivyake sera, miongozo na kanuni na mapendekezo ya kufikia malengo ya kukabiliana na ufisadi, kuboresha utoaji huduma na uwajibikaji wa taasisi za mihimili yote ya serikali kwa watu wa Kenya.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakati wa mkutano huo, ilikubaliwa kwamba ndani ya siku 30, kila mhimili wa serikali utawasilisha mapendekezo hayo kwa kongamano la Baraza la Kitaifa la Utawala wa Sheria (NCAJ) litakaloitishwa na Jaji Mkuu Koome.

“Kongamano hili litatoa mwongozo wa hatua za kuchukuliwa mara moja, kwa muda wa kati na muda mrefu,” inaongeza taarifa hiyo.

Na ili kuhakikisha utoaji bora wa huduma na kuimarisha vita dhidi ya ufisadi, serikali kuu na bunge zitaunga mkono ombi la idara ya mahakama kutengewa fedha zaidi ili kusaidia miongoni mwa mambo mengine kuajiriwa kwa majaji wapya 25 wa mahakama kuu na majaji wapya 11 wa mahakama ya rufaa.

Serikali kuu, bunge na idara ya mahakama zikiahidi kuzika tofauti kati yao na kufanya kazi katika hali inayoheshimu, kukuza na kuheshimu utawala wa sheria, kuheshimu uhuru wa kila asasi na kuheshimu maamuzi ya mahakama.

Hayo yanakuja siku chache baada ya vita vya maneno kuzuka kati ya serikali kuu na idara ya mahakama.

Rais William Ruto katika siku za hivi majuzi amekuwa akiikosoa idara ya mahakama kwa kushirikiana na watu fulani kuhujumu miradi ya serikali, akitaja maagizo yanayotolewa mara kwa mara kuzuia utekelezaji wa miradi hiyo.

Ametoa mfano wa mradi wa nyumba za gharama nafuu na upatikanaji wa afya kwa wote.

Ruto alihusisha hali hiyo na kukithiri kwa ufisadi katika idara ya mahakama, hali iliyomchochea Jaji Mkuu Koome kuitisha kikao cha kuangazia madai hayo na kutafuta njia mwafaka ya kutatua masuala yaliyoibuliwa.

Muungano wa Azimio na chama cha wanasheria nchini, LSK walipinga kufanyika kwa mkutano kati ya Rais Ruto na Jaji Koome wakihofia huenda ukaathiri utendakazi wa idara ya mahakama.