Home Kaunti Visa vya mauaji vyaongezeka Nyahururu

Visa vya mauaji vyaongezeka Nyahururu

0

Wakazi wa mji wa Nyahururu wanaishi na hofu kufuatia kuongezeka kwa visa vya mauaji mjini humo na maeneo ya karibu.

Mwendesha bodaboda alishambuliwa na majambazi walokuwa wamejihami waliomwacha na majeraha na kumpokonya pikipiki yake katika kijiji cha Silale karibu na mji wa Nyahururu.

Mwanablogu Bob Ojare maarufu kama Bobby Bobby naye aliaga dunia baada ya kushambuliwa na wezi katika eneo lake la kazi mjini Nyahururu na wakamwacha na majeraha mabaya ya kichwa yaliyosababisha kifo chake.

Wezi hao waliingia kwenye chumba alichokuwa Bobby wakakata nyaya za kamera za CCTV kabla ya kumshambulia. Walimvua nguo, wakachukua simu, pesa, redio, pombe, kuku na mashine ya pesa.

Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Nyahururu na uchunguzi unaendelea ili kukamata na kuwashtaki wahusika.

Kando na visa hivyo viwili, makanisa, maduka na nyumba za makazi zimekuwa zikivamiwa na wezi ambao wamejihami suala linalolazimisha wengi kufunga biashara mapema.

Naibu Kamishna wa kaunti Joseph Kanyiri, amehakikishia wakazi wa eneo hilo usalama akisema maafisa wa usalama wanaendeleza uchunguzi ili kukamata wezi hao.

Kanyiri aliongeza kwamba kamati ya ulinzi katika eneo hilo itashirikiana na wakazi kutafuta suluhisho kwa tatizo hilo huku akiwaomba kutoa habari zinazoweza kufanikisha kukamatwa kwa wezi hao.

Website | + posts