Home Taifa Viongozi watakiwa kuunga mkono juhudi za kuwaunganisha Wakenya

Viongozi watakiwa kuunga mkono juhudi za kuwaunganisha Wakenya

0
kra

Rais William Ruto ametoa wito kwa viongozi kutoka mirengo mbalimbali ya kisiasa kuunga mkono jitihada zinazoendelea za kuwaunganisha Wakenya kwa ajili ya umoja na maendeleo ya nchi. 

Ruto amewasihi viongozi wasiounga mkono serikali jumuishi kufanya hivyo kwa misingi ya uzalendo.

kra

Amesema umoja na maendeleo ya nchi ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya kibinafsi na ya kisiasa ya viongozi.

“Nataka kuwaambia viongozi wenzangu kwamba huu si wakati wa sisi kuwa na migawanyiko, kufikiria juu ya maslahi ya kibinafsi au mirengo ya kisiasa. Huu ni wakati wa kufikiria juu ya Kenya,” alisema Ruto wakati ziara yake ya siku tatu katika kaunti za Kisii na Nyamira ikiingia siku ya pili leo Jumanne.

“Hebu tufanye kazi sote pamoja kuelekea mabadiliko, maendeleo na umoja ili tuweze kuupiga umaskini dafrau.”

Rais Ruto siku chache zilizopita aliteua Baraza Jipya la Mawaziri linalojumuisha wanachama wa upinzani katika juhudi za kuliunganisha taifa.

Wale walioteuliwa kuwa mawaziri kutoka chama cha ODM ni John Mbadi (Fedha), Opiyo Wandayi (Nishati), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika) na Hassan Joho (Madini).

Hatua ya wanachama wa ODM kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza imekosolewa vikali na baadhi ya viongozi wa muungano wa upinzani wa Azimio akiwemo Kalonzo Musyoka na Eugene Wamalwa ambao wameitaja kuwa ya kuwasaliti Wakenya.

ODM ni chama tanzu cha muungano wa Azimio.