Home Kimataifa Viongozi waombwa watangulize maslahi ya Wakenya

Viongozi waombwa watangulize maslahi ya Wakenya

0
Gavana wa kaunti ya Kakamega, Fernandes Barasa.
Gavana wa kaunti ya Kakamega, Fernandes Barasa.
kra

Viongozi walioteuliwa kuwakilisha mirengo ya kisiasa ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja One Kenya kwenye mazungumzo ya maridhiano wameombwa watangulize maslahi ya Wakenya wote kwenye mazungumzo hayo yanayotarajiwa kuanza wiki hii.

Haya yanajiri wakati ambapo kila mrengo unalaumu mwingine kwa kujaribu kuhujumu mazungumzo hayo.

kra

Gavana wa kaunti ya Kakamega Fernandes Barasa ameomba wawakilishi wa mirengo yote kwenye mazungumzo hayo watoe kipaumbele kwa mambo ambayo yanawakumba Wakenya wote.

Barasa alikuwa akizungumza katika eneo bunge la Malava ambapo alisisitiza umuhimu wa uwazi wakati wa mazungumzo hayo huku akisihi wanasiasa kuweka kando tofauti zao za kisiasa.

Huku haya yakijiri, wabunge wa mrengo wa Azimio kutoka eneo la Pwani wamelaumu wenzao wa mrengo wa Kenya Kwanza kwa kile walichokitaja kuwa kutokuwa wakweli.

Mrengo wa azimio umewateua kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa wachache katika bunge la taifa Opiyo Wandayi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni na mbunge wa Malindi Amina Mnyanzi kama wawakilishi wake kwenye mazungumzo hayo.

Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah, kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Aaron Cheruiyot, Gavana wa Embu Cecily Mbarire, mbunge wa bunge la Afrika Mashariki, EALA Hassan Omar na mwakilishi wa kaunti ya Bungoma Catherine Wambilianga ndio wanaowakilisha mrengo wa Kenya Kwanza.

Ripoti yake Giverson Maina

Website | + posts