Home Habari Kuu Viongozi Wajir wataka usaidizi wa serikali kuu kukabiliana na athari za El...

Viongozi Wajir wataka usaidizi wa serikali kuu kukabiliana na athari za El Nino

0

Viongozi wa kaunti ya Wajir wanaomba usaidizi wa serikali kuu katika kukabiliana na athari za mvua ya El Nino inayoendelea kushuhudiwa nchini.

Wakiongozwa na Gavana Ahmed Abdullahi, viongozi hao walielezea kwamba maji ya mafuriko yamezingira makazi ya familia kadhaa huku mifugo wakikwama kwenye matope.

“Kabla ya mvua ya El Nino kuanza, serikali za kaunti ziliomba shilingi bilioni 15 za kukabiliana na athari za mvua. Sijui kama kuna kaunti imepokea fedha hizo.” alisema Gavana huyo.

Alisema kiwango cha maji ya mvua ya sasa ni mara 20 ya kiwango cha kawaida na kwamba mengine yanatoka Ethiopia na sehemu za kati mwa nchi.

Abdullahi aliongeza kwamba barabara zote za kuelekea kaunti ya Wajir hazipitiki na usafirishaji wa chakula na dawa umeshindikana.

Kulingana naye, tani 57 za dawa zimekwamba barabarani tangu wiki jana huku akiahidi kwamba serikali yake itafanya kila juhudi kushughulikia hali hiyo.

Aliomba usaidizi kutoka kwa wadau mbali mbali yakiwemo mashirika ya misaada.

Mbunge wa Eldas Adan Keynan kwa upande wake alisema iwapo mvua ya El Nino itaendelea kunyesha kwa mwezi mmoja, barabara zitaharibiwa kabisa.

Alitaka ndege zitolewe ili kusafirisha chakula na dawa kwa wanaozihitaji katika maeneo yaliyoathirika.

Seneta Abass Sheikh alishangaa ni kwa nini serikali inaangazia maeneo kama Mombasa huku ikikosa kuhudumia eneo la kaskazini mwa nchi.

Kiongozi huyo alisema hata ingawa kampuni ya usafiri wa ndege ya Blue Bird Aviation imejitolea kusafirisha dawa na chakula bila malipo, vitu hivyo huenda visifikie walengwa kutoka uwanja wa ndege wa Wajir.

Fatuma Jehow Abdi mwakilishi wa kaunti ya Wajir bungeni aliangazia ukosefu wa mafuta katika eneo hilo hali ambayo huenda ikakatiza mawasiliano kufikia Ijumaa.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza wakati wa kuzindua tani 24 za dawa zilizonunuliwa na serikali ya kaunti kutoka kwa kampuni ya Kemsa.

Viongozi wengine waliokuwepo ni mbunge wa Tarbaj Hussein Barre, Adan Daud wa Wajir mashariki na Yusuf Farah wa Wajir magharibi.

Website | + posts