Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi ambaye pia ni waziri wa masuala ya nchi za kigeni amewataka viongozi kujiepusha na siasa za kikabila.
Mudavadi aliyekuwa akizungumza katika shule ya wasichana ya Chepterwai huko Mosop, kaunti ya Nandi alisema kwamba hiyo ndiyo njia ya kuhakikisha umoja humu nchini.
Akihutubia waliohudhuria hafla ya kutoa shukrani shuleni humo, waziri Mudavadi alisema kwamba viongozi hawafai kuangazia za kikabila ambazo huenda zikairejesha nchi hii kwa siku mbaya.
Kiongozi huyo ambaye alimwakilisha Rais William Ruto kwenye hafla hiyo alisisitiza kwamba serikali imejitolea kubadilisha nchi hii, ambapo aliongeza kwamba wanaoishi karibu na vyanzo vya maji watahamishwa kwa usalama wao.
Kulingana naye bunge limetenga shilingi bilioni 9 za kushughulikia madhara yaliyotokana na mafuriko ya hivi maajuzi.
Mudavadi alionya mawaziri dhidi ya matamshi ambayo huenda yakachukuliwa kuwa msimamo wa serikali.
Kuhusu elimu, waziri aliye na mamlaka makuu alisema kwamba serikali imejitolea kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata elimu kupitia mpango thabiti wa ufadhili wa taasisi za elimu.
Alitaja pia mipango ya kuboresha mazingira katika taasisi za elimu kwa lengo la kukuza talanta za wanafunzi na kuchochea ubunifu.