Home Habari Kuu Viongozi wa kidini wasema wako tayari kupatanisha serikali na upinzani

Viongozi wa kidini wasema wako tayari kupatanisha serikali na upinzani

0

Askofu mkuu wa jimbo kuu la Nairobi la kanisa Katoliki Philip Anyolo anasema kwamba viongozi wa kidini sasa wako tayari kupatanisha Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Anyolo alifichua kwamba kundi la viongozi wa dini mbalimbali liko tayari kuongoza mazungumzo kati ya viongozi hao wawili huku mgawanyiko kati yao ukizidi kuongezeka.

Anyolo, hata hivyo, anatambua kwamba viongozi wa kidini hawawezi kufanikisha hilo iwapo Rais Ruto na Raila hawako tayari kupatanishwa. Anahisi kwamba uhasama kati ya wawili hao huenda ukasababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini kati ya wafuasi wao.

Akizungumza katika kanisa la mtakatifu Bernadette katika eneo la Ngoingwa, Thika, kaunti ya Kiambu, Anyolo alilaani maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea katika sehemu mbalimbali za nchi akisema huenda yakazidi na kusababisha machafuko.

Huku upande wa upinzani ukiendelea kuruhusiwa kujieleza kupitia maandamano, Anyolo anahisi wafuasi wa mrengo huo hawafai kukiuka haki za Wakenya wengine kupitia kuharibu mali ya umma na ya kibinafsi.

Amesema kutokana na hali ilivyo, Wakenya walio na njaa wamekuwa wakimiminika kwenye makanisa ya Katoliki katika kaunti ya Nairobi kuomba chakula. Anasema kanisa halina uwezo wa kuendelea kutoa misaada ya chakula kwa Wakenya wanaokumbwa na njaa.

Kiongozi huyo wa kidini anataka serikali imakinike na ishughulikie changamoto wanazopitia Wakenya hasa gharama ya juu ya maisha kama njia ya kutuliza mvutano unaoendelea.

Mbunge wa Thika Alice Ng’ang’a aliyehudhuria ibada hiyo, aliwataka waumini kuombea nchi hii kabla ya maandamano yanayopangiwa kufanyika Jumatano, Alhamisi na Ijumaa wiki hii.

Ripoti yake Antony Kioko

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here