Home Kimataifa Viongozi wa kidini wakamatwa nchini Tanzania kwa kuwazuilia wagonjwa

Viongozi wa kidini wakamatwa nchini Tanzania kwa kuwazuilia wagonjwa

0

Viongozi wawili wa kidini wametiwa nguvuni nchini Tanzania kwa madai ya kuwazuilia wagonjwa.

Wawili hao walikamatwa wakati ulimwengu ukiendelea kusikitikia kufukuliwa kwa mamia ya miili kutoka kwenye makaburi ya halaiki inayoaminiwa kuwa ya wafuasi wa kanisa la Good News International linaloongozwa na mhubiri Paul Mackenzie.

Kulingana na maafisa nchini humo, viongozi hao wawili waliahidi wagonjwa hao kuwa watawaponya kwa maombi na kupitia matibabu ya dawa za kienyeji.

Watu zaidi ya 100, ambao walikuwa wamewekwa katika nyumba moja katika kijiji cha Nyamhinza, wilayani Misungwi bila chakula wala matibabu, waliokolewa na maafisa hao baada ya wananchi kuwapasha polisi habari.

Inaaminika kuwa wagonjwa wengine walikuwa wamekaa huko kwa muda wa mwezi mmoja, na walitakiwa kujitafutia chakula hadi wapone kabisa.

Kulingana na wananchi, watu hufariki wanapotoka hospitalini, wa hivi karibuni akiwa mwanamke aliyejifungua pacha.

Aidha polisi wanachunguza vifo ambavyo huenda vilitokea na ikiwa kuna miili iliyozikwa hivi karibuni.

Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, aliwaambia waandishi wa habari jana Jumatano kuwa uchunguzi wa awali haukuonyesha kulikuwa na watu waliozikwa humo lakini wanaendelea kufuatilia kwa karibu.

Alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, viongozi wa kanisa hilo William Masum na mkewe Kabula Lushika, akisema hawakuwa na vibali vya kuendesha ibada na maombi, wala kutoa huduma za tiba asilia.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here