Home Habari Kuu Viongozi wa Kenya Kwanza wamsuta Uhuru

Viongozi wa Kenya Kwanza wamsuta Uhuru

0
Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwa muda amekuwa akilaumiwa na viongozi wanaoegemea utawala wa Kenya Kwanza. 
Wakosoaji wake wakidai kuwa alichangia, kwa kiwango kikubwa tu, matatizo ya kiuchumi yanayoikabili nchi hii kwa sasa.
Hususan, wanamtuhumu kutokana na hulka yake ya kukopa madeni chungu nzima wakati wa utawala wake, madeni ambayo yamefanya iwe vigumu kuiendesha nchi.
Na sasa kiwango kikubwa cha kodi inayokusanywa kinatumiwa kulipa madeni yaliyokopwa na utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, wanasema viongozi hao, hali ambayo pia imechangia gharama ya maisha kuwa ya juu zaidi.
Ni shutuma ambazo zilimfanya Rais Mstaafu kuvunja kimya chake Jumapili iliyopita.
Kenyatta akiukosoa utawala wa Rais Ruto kwa kutumia muda mwingi kumnyoshea kidole cha lawama badala kutimiza ahadi walizotoa kwa Wakenya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
“Hata wengine wakishindwa kupata watoto, watadai ni mimi niliyesababisha,” alisema Rais Mstaafu wakati akiwahutubia waumini katika kanisa moja eneo la Mwingi.
Ni kauli ambazo bado zinaendelea kukemewa na baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza.
Wakiongozwa na Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na Gavana wa Nandi Stephen Sang, walidai utawala uliopita ulisimamia ubadhirifu wa rasilimali za umma na kukopa madeni kupita kiasi.
Sasa wanamtaka Rais Mstaafu kufyata mdomo na kujionea mwenyewe wakati serikali ya Kenya Kwanza ikitimiza ahadi zake kwa Wakenya.
Viongozi hao waliyasema hayo katika eneo la Mosoriot, kaunti ya Nandi.
Martin Mwanje & Kimutai Murisha
+ posts